Baada ya taarifa ya jeshi kutangazwa, waandamanaji wanaopinga Bw Morsi ambao walikuwa wamekusanyika katika uwanja wa Tahrir na karibu na Ikulu mjini Cairo walisherehekea uamuzi huo. Mwandamanaji mmoja Ashraf Seif alifurahia uamuzi huo wa jeshi, alisema,
"hatua ya jeshi ni nzuri na ya kizalendo. Katika mwaka mmoja wa rais Morsi na Chama cha Muslim Brotherhood kuwa madarakani, walijali tu kudhibiti jeshi, idara za utekelezaji wa sheria na idara zote za serikali, na kuifanya nchi idhibitiwe na Chama cha Muslim Brotherhood. Watu wote wa Misri waliona kuwa uchumi wa nchi unaporomoka kwa kasi sana.
Lakini si watu wote wanafurahia kuondolewa madarakani kwa rais Morsi na kipindi cha mpito kinachoongozwa na jeshi. Bibi Sahran Ibrahimu alionesha wasiwasi wake,
"Tunaunga mkono nchi kuwa ya kawaida, tunapinga utawala wa Chama cha Muslim Brotherhood, pia tunapinga utawala wa kijeshi. Hayo ni matakwa ya kimsingi ya wananchi wa Misri."
Mwandishi maarufu wa habari wa Misri Bw. Hossein Ismail alisema jeshi la Misri lilichukua hatua jumatano usiku kwa sababu usalama wa nchi uko hatarini, ndiyo maana si mapinduzi ya kijeshi, tena jeshi hilo halina nia ya kuanzisha utawala wa kijeshi.
"Jeshi liliwaita viongozi wote wa kikabila na kidini kuhudhuria mkutano, na kutoa taarifa kwa mujibu wa maoni ya viongozi hao. Hii ni ishara kwa dunia nzima hasa wananchi wa Misri kuwa, jeshi halina nia ya kuingilia mambo ya siasa."
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Cairo Bw. Jaber Nassar alisema kutokana na katiba kusimamishwa, rais wa muda Adli Mansour atatawala nchi kwa kutoa taarifa za katiba, na kutekeleza mpango wa mpito ukiwemo kuitisha uchaguzi mkuu mapema na kuhimiza masikilizano ya kitaifa. Baada ya katiba mpya kutungwa, utawala wa kisheria na uwiano kati ya makundi mbalimbali ya kisiasa utarudishwa nchini humo, na jeshi halitadhibiti mambo ya siasa. Pia alisema uchaguzi wa rais unatazamiwa kufanyika ndani ya mwaka mmoja.
"Tume ya utungaji wa katiba ikiundwa na watu huru maarufu, itamaliza kazi yake ndani ya muda mfupi. Baadaye uchaguzi wa bunge na rais utafanyika. Kazi hizo zinaweza kumalizika ndani ya miezi 9 hadi 12."
Chama cha Muslin Brotherhood na tawi lake Chama cha Freedom and Justice viliingia madarakani baada ya rais wa zamani Hosni Mubarak kuondolewa madarakani. Baada ya mwaka mmoja, rais Morsi pia ameondolewa madarakani. Watu wana matarajio na wasiwasi kuhusu Chama cha Muslin Brotherhood kitakuwa na mustakbali gani. Bw. Hossein Ismail alisema,
"Chama cha Muslin Brotherhood kitakuwa na njia mbili katika siku zijazo. Njia ya kwanza ni kushiriki mchakato wa kisiasa kupitia tawi lake la Chama cha Freedom and Justice. Kwa sasa bado kina fursa ya kufuata njia hii. Na njia nyingine ni kutekeleza siasa kali na kutumia mabavu, njia ambayo naona haitakisaidia. Tukiangalia historia ya Misri, majaribio yote ya kimabavu ya makundi yenye siasa kali yameshindwa."
Baada ya jeshi la Misri kutoa taarifa, mapambano kati ya watu wanaomwunga mkono Rais Mohamed Morsi na wanaompinga yalitokea katika sehemu mbalimbali. Alhamisi Chama cha Muslin Brotherhood kilitoa wito kuwataka wafuasi wake kufanya maandamano ya amani. Lini utulivu utarudishwa nchini Misri, hii bado haijulikani.